Lema atiwa mbaroni, Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa Mbunge Tundu Lisssu

WAKATI Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kwa sababu amekiuka masharti ya dhamana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amekamatwa na Polisi kwa mahojiano ya kutoa lugha za uchochezi.
Lema alikamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa mkoani Dodoma, kuhudhuria vikao vya Bunge na kusafirishwa hadi Arusha.

Godbless Lema


Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Charles Mkumbo, alisema Lema yuko mahabusu kwa mahojiano mpaka watakapomaliza na kumfikisha mahakamani, kujibu makosa anayokabiliwa nayo.

Mkumbo alisema Lema amekuwa akitoa maneno na lugha za uchochezi na kuzirudia kila mara, hivyo wameona vyema wamweke ndani kwa mahojiano. “Juzi tulimkamata akitokea Dodoma na tulifanya naye mahojiano na kumwachia kwa dhamana, lakini kuna baadhi ya makosa hatukuwahi kumhoji, sasa ndio tumeamua kumhoji,” alisema.

Pamoja na Polisi kutosema ni lugha gani ya uchochezi imetumiwa na Mbunge huyo kiasi cha kuka matwa, Novemba Mosi mwaka huu Kamanda Mkumbo akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alitaja maneno ya uchochezi anayodaiwa kuyasema Lema.

Alisema kwamba Lema alitamka maneno haya: “Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiendelea kukandamiza demokrasia na siasa za ukandamizaji, taifa litaingia katika umwagaji wa damu, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta”. Wakati mbunge huyo anahojiwa na Polisi mjini Arusha, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, amelaani kukamatwa kwa mbunge huyo, akidai ni utekaji nyara.

Katika kesi inayomhusu Tundu Lissu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba wa Mahakama ya Kisutu alitoa hati ya kukamatwa kwa mbunge huyo wa Chadema kwa sababu amekiuka masharti ya dhamana katika kesi ya uchochezi, inayomkabili na wenzake watatu. 

#HabariLeo