Singida. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria madereva wanaoacha mawe na matawi ya miti barabarani.
Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi alitoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha 38 cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Singida. Alisema baadhi ya madereva wa magari na hasa makubwa hutumia mawe kuyazuia kutembea wanapofanya matengenezo ya dharura na wanapomaliza huyaacha barabarani.
“Wakishamaliza matengenezo madereva huyaacha barabarani mawe na matawi ya miti ambayo hutumika kutoa tahadhari kwa vyombo vingine vya moto. Kitendo hicho kinahatarisha maisha na mali za watumiaji wengine wa barabara kwa vile yanaweza kusababisha ajali,” alisema Mwigulu na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linapaswa kuimarisha mawasiliano ili kuwadhibiti na kuwakamata madereva hao.
Pia, alisema kuna umuhimu wa wananchi na hasa wanaoishi kando ya barabara kuelimishwa kuhusu matumizi bora ya barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi ili waache kupitisha mifugo na mikokoteni barabarani. Mwenyekiti wa bodi hiyo, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe aliagiza fedha zinazotolewa na Serikali na wafadhili kwa ajili ya miradi ya barabara, matumizi yake yasimamiwe kikamilifu ili zitumike kwa miradi iliyokusudiwa.
“Ujenzi wa miradi ufanane na thamani halisi ya fedha zilizotumika. Makandarasi bora na wenye uwezo wa kutekeleza miradi ndiyo wapewe kazi ili kuzikamilisha kwa wakati,” alisema Mtigumwe.
Alisisitiza kuimarishwa kwa usimamizi na ukaguzi wa mara kwa mara wa miradi ya barabara ili ziwe za kiwango bora.
Mhandisi Mtigumwe ambaye kabla ya uteuzi wa ukuu wa mkoa alikuwa meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads)wa mkoa, aliupongeza uongozi wa wakala huo Singida chini ya Meneja, Injinia Leonard Kapongo kwa kazi ya usimamizi na ukaguzi uliowezesha miradi ya barabara kujengwa kwa ubora unaofafana na fedha zilizotumika.