Samia Suluhu: Serikali inajipanga kuondoa utitiri wa kodi zinazotozwa kwenye viwanda

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inajipanga kuondoa utitiri wa kodi mbalimbali zinatozwa kwenye viwanda kama hatua ya kuviwezesha viwanda vingi nchini  kuongeza uzalishaji na kutoa ajira nyingi kwa watanzania.

Samia Suluhu


Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo leo Jijini Arusha baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kupikia cha Mount Meru Millers ili kujua changamoto zinazokikabili kiwanda hicho ili Serikali iweze kuzifanyia kazi katika kuleta unafuu kwenye uzalishaji wa mafuta ya kupikia nchini.

Makamu wa Rais amesema mlolongo wa kodi zinazotozwa kwa wamiliki wa viwanda hazina uratibu mzuri hivyo mkakati ya Serikali wa awamu ya Tano inataka kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa kodi hizo ikiwemo kuondoa kodi ambazo ni kero kwenye viwanda.

Amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha viwanda vingi vinajengwa nchini ambavyo vitatumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini hali ambayo itasaidia uuzaji wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kuuzwa kwenye masoko ya nje ya nchi na kuliingizia taifa mapato na kuongeza ajira kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema ziara ambazo anafanya kwenye viwanda mkoani Arusha ni kujionea jinsi viwanda hivyo vinavyofanya kazi za uzalishaji na pale kwenye changamoto zinazokwamisha viwanda hivyo kufanya kazi vizuri ziweze kufanyia kazi na Serikali. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mount Meru Millers Atul Mittal amesema kama Serikali itafuta au kuondoa utitiri wa kodi wanazotozwa kwenye Viwanda hivyo watakuwa na uwezo wa kuongeza maradufu uzalishaji na kutoa ajira nyingi kwa Watanzania.

Amesema kwa sasa Kampuni hiyo inafanya kazi kwenye nchi 10 barani Afrika na kwa Tanzania pekee imeajiri wafanyakazi zaidi ya 1000 ambao wanafanyakazi katika maeneo mbalimbali nchini.