SERIKALI HAINA IDADI YA WATANZANIA WATAKAOTIMULIWA NA TRUMP MAREKANI

Dar es Salaam. Serikali imesema kuna Watanzania wengi wanaoishi Marekani kinyume cha sheria, lakini haijui idadi yao wakati Rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump akisubiriwa kutekeleza ahadi yake ya kutimua wahamiaji haramu.



Kuchaguliwa kwa Trump kuwa Rais wa 45 wa Taifa hilo kubwa, kumeibua hofu miongoni mwa kwa mataifa mbalimbali kuhusu raia wao wanaoishi bila ya nyaraka halali kutokana na sera za mfanyabiashara huyo maarufu za kutotaka wageni haramu.

Awali, Serikali ya Rais Barack Obama ilitoa ahueni kwa watu wanaosadikiwa kuwa milioni 11.1 (kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014 za taasisi ya utafiti ya Pew ya Marekani) baada ya kuwaruhusu kupitia mchakato ambao ungewapa uhalali wa kuishi nchini humo.

Lakini katika kampeni zake, Trump alisema hahitaji wageni walioingia Marekani kwa kukwepa sheria na hivyo atawatimua ili wakaanze mchakato wa kuomba kuingia Marekani wakiwa kwenye nchi zao.

Akizungumza na Mwananchi juzi, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje, Robi Bwiru alisema: “Kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi Marekani lakini kwa kuwa suala la mtu kutaka kutambulika na ubalozi wake ni la hiari, hatuna idadi kamili ya Watanzania ambao wapo kule bila nyaraka halali.” Kuhusu misimamo ya kiongozi huyo kutoka chama cha Republican dhidi ya nchi za Afrika, Bwiru alisema Tanzania haiwezi kutoa msimamo wowote kabla ya kuona utekelezaji wa ahadi zake. 

#mwananchi