Serikali kutumia trilioni 32.9/- mwaka 2017/2018 (Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa)

SERIKALI imepanga kutumia Sh trilioni 32.946 katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018, ikiwa imeongezeka kutoka Sh trilioni 29.5 ya mwaka 2016/2017 na kutaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na kuzingatia miradi ya kufufua kiwanda cha General Tyre cha Arusha na kuendeleza maeneo ya viwanda vidogo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango


Sambamba na hilo, serikali imebainisha mikakati yake ya kudhibiti matumizi, ambapo sasa itahakikisha mikataba inayoingiwa na serikali na taasisi zake inakuwa katika shilingi za Tanzania, isipokuwa kwa mikataba inayohusisha biashara za kimataifa.

Kuhusu kuhamishia shughuli za makao makuu ya serikali Dodoma, mipango ya ujenzi wa majengo na miundombinu yote ya serikali iliyopangwa kujengwa Dar es Salaam, itahamishiwa Dodoma.

Akiwasilisha bungeni jana mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka 2017/2018, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kati ya Sh trilioni 32.946, Sh trilioni 19.782 zitatengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. “Sh trilioni 7.206 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma na Sh trilioni 9.723 ni kwa ajili ya kulipia deni la Taifa lililoiva. Matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 13.164 sawa na asilimia 40 ya bajeti yote ambapo fedha za ndani ni Sh 9.960 sawa na asilimia 76. Kiwango hiki ni ongezeko la Sh trilioni 1.343 ikilinganishwa na mwaka 2016/2017,” alifafanua.

Alisema mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 20.872 sawa na asilimia 63 ya mahitaji yote.
Kati ya mapato hayo serikali inatarajia kukusanya mapato ya kodi ya Sh trilioni 18.097 sawa na asilimia 87 ya mapato ya ndani.

#HabariLeo