Vyama vya Siasa Vitatu Vyafutwa vya Mapalala, Mziray vyafutwa

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amefuta usajili wa kudumu wa vyama vya siasa vitatu kutokana na kupoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa.

Vyama hivyo ni Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA), The African Progressive Party of Tanzania (APPT-Maendeleo) na Jahazi Asilia.



Chausta ni chama kilichopata usajili wa kudumu Novemba 15, 2001 na kilikuwa kinaongozwa na James Mapalala akiwa Mwenyekiti, APPT - Maendeleo kilipata usajili Machi 4, 2003 kikiongozwa na Peter Mziray kama Rais Mtendaji wakati Jahazi Asilia kilipata usajili Novemba 17, 2004 na Mwenyekiti wake ni Kassim Bakari Ali.

Kufutwa kwa vyama hivyo vitatu, kunaifanya Tanzania ibaki na vyama 19 vyenye usajili wa kudumu, kwa mujibu wa orodha ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Jaji Mutungi alisema kila chama kilipewa taarifa ya nia ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuta usajili wa kudumu na kutakiwa kueleza kwa nini kisifutwe.

Alieleza kuwa katika utetezi wao, vyama hivyo vilishindwa kutoa sababu za kuridhisha kuwa havijakiuka sheria na bado vinazo sifa za usajili wa kudumu.

Jaji Mutungi alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi kuhusu hatua hiyo na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 7( 3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, taasisi yoyote hairuhusiwi kufanya kazi kama chama cha siasa, kama haijasajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa. “Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya Mwaka 1992, nimefuta usajili wa kudumu wa vyama vya siasa vitatu kuanzia leo (jana),” alisema Jaji Mutungi.

#HabariLeo