Mwanachuo Udom aachiwa huru

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imetengua uamuzi wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ya kumfukuza mwanachuo Phillip Mwakibinga na kuamuru arudishwe ili kumalizia masomo yake.



Uamuzi huo ulitolewa jana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, John Chaba kwa niaba ya Jaji Awadhi Mohamed aliyekuwa akisikiliza shauri hilo.

Mwakibinga alikuwa akisoma Shahada ya Kiswahili mwaka wa tatu wakati akisimamishwa na alikuwa Waziri Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii. Katika uamuzi huo, mahakama ilisema mlalamikaji hakupewa nafasi ya kusikilizwa na hivyo kukiuka haki ya asili ya mlalamikaji. Pia mlalamikaji hakupewa haki ya kusikilizwa na hakuandikiwa mashtaka rasmi. “Baraza liliegemea upande moja bila kumhoji wala nafasi ya kusikilizwa na kujitetea,” alisema. Mwakibinga alifukuzwa Udom Januari 14, mwaka jana, kwa madai ya kuongoza mgomo ambapo siku hiyo baraza la chuo lilikaa na kumfukuza bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.

Alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kutaka mahakama kutengua uamuzi huo. Kwa mujibu wa wakili wa Mwakibinga, Elias Machibya alisema awali waliomba ruhusa ya kufungua kesi na wakapewa Februari 5, mwaka jana wakiomba kutengua maombi ya baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma. 

#HabariLeo