POLEPOLE: BADO NAAMINI MUUNDO WA SERIKALI TATU

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amesema hawezi kupindisha maneno kuhusu msimamo wake wa muundo wa Serikali tatu.

Polepole na Nape


Polepole alikuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, ambao pamoja na mambo mengine, waliridhia uwapo wa muundo wa Serikali tatu ambazo ni Serikali ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba, Dar es Salaam jana, Polepole alisema ataendelea kusimamia hoja yake. “Siwezi kupindisha maneno yangu kuhusu muundo wa Serikali tatu katika Katiba mpya, nitaendelea na kusimamia hoja yangu kama nilivyokuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. “Kama kuna watu wanataka kubadilisha hoja ya CCM katika kipindi hiki ambacho kinasimamia kuleta maendeleo kwa wananchi, hawatafanikiwa. “Tutaendelea kuwatumikia wananchi kama ilivyokuwa kwenye ilani ya CCM wakati chama hiki kinaanzishwa, muda wa siasa za madaraka umekwisha baada ya kumalizika uchaguzi mkuu mwaka jana,” alisema Polepole.

Alisema pamoja na kuwapo mabadiliko ya wajumbe wa Kamati Kuu yaliyotangazwa hivi karibuni na Rais Dk. John Magufuli, CCM itaendelea na misimamo yake kama ilivyokuwa kwenye misingi ya uanzishwaji wake. “Kuanzia sasa, CCM itarudi katika misingi yake, ikiwa ni pamoja na kuwatumikia wananchi bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, dini wala rangi,” alisema.

Kuhusu nafasi yake ya ukuu wa wilaya, Polepole alisema hadi sasa hajapewa barua ya kutenguliwa nafasi hiyo.

Polepole alisema kuwa alimuomba Rais Magufuli kumpa mwezi mmoja ili aweze kumaliza kero za wananchi wa Wilaya ya Ubungo, kwa sababu wana migogoro mingi, ikiwamo ya ardhi.

Alisema anatamani kumaliza kero hizo ili aweze kuondoka bila ya kuwa na deni, jambo ambalo linaweza kumpa sifa Rais Magufuli na Serikali yake kuliko akiondoka sasa hivi wakati wananchi bado wana malalamiko. 

#Mtanzania