‘Scorpion’ uso kwa uso na anayedaiwa kumtoboa macho

KWA mara ya kwanza mshitakiwa katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi, Salum Njwete maarufu Scorpion, amekutana na mlalamikaji katika kesi hiyo, Said Mrisho katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, iliposikilizwa jana.



Mrisho, ambaye ndiye shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, aliieleza mahakama hiyo kuwa alichomwa visu tumboni na mgongoni kabla ya kutobolewa macho.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule, Mrisho alidai kuwa wakati tukio hilo linaendelea, alimkariri mshitakiwa kwa kumuangalia usoni.

Akielezea tukio lilivyotokea, alidai Septemba 6, mwaka huu saa nne usiku alikuwa kazini kwake Tabata Segerea kwa kazi yake ya kinyozi na baada ya kufunga ofisi, alikwenda kituoni kusubiri usafiri wa kwenda nyumbani kwake Makuburi, karibu na Ubungo.

Kabla ya kuanza kutoa ushahidi huo, mshitakiwa ambaye alipandishwa kizimbani saa 3.35 asubuhi, aliomba mahakama isianze kusikiliza shauri hilo hadi wakili wake wa utetezi afike. Mahakama hiyo ilikubaliana na ombi hilo, ambapo baada ya dakika 15 kupita wakili alifika na kuanza na usikilizwaji.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa ambaye ni mwalimu wa karate, alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala.

Ilidaiwa mshitakiwa aliiba cheni ya dhahabu gramu 38 yenye thamani Sh 60,000, kibangili cha mkononi na Sh 331,000 pamoja na pochi, vyote vina thamani ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.

Ilidaiwa kabla ya wizi huo, alimchoma na kisu tumboni mgongoni na machoni. Kesi hiyo itaendelea na ushahidi Desemba 28, mwaka huu na mshitakiwa alirudishwa rumande. 

#HabariLeo