Serikali kuendelea kutibu sumu ya nyoka

SERIKALI imesema itaendelea kutoa dawa zinazotibu sumu ya nyoka ili kupambana na tatizo hilo nchini. Kauli hiyo ya serikali ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. “Kama tunavyofahamu nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.” Alisema dawa za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi; na kwamba si tu hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa.



Waziri huyo alisema bei ya kununulia dawa hizo ni kati ya dola za Marekani 55 hadi 85 (yaani Sh 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo kimoja.

Alisema kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja tu.

Waziri alisema pamoja na changamoto hizo, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kila mwaka huagiza dawa hizo kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni Sh 200,000 kwa kichupa kimoja. “Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa wasambazaji wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika. “Napenda kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za tiba hutolewa bure kwa makundi maalumu au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya gharama, au kwa kupitia mfumo wa bima mbalimbali za afya kama vile CHF. “Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu wa msamaha hutumika,” alisema Waziri.

#HabariLeo