MGOMO WA WACHEZAJI YANGA WALETA SARE NA AFRIK LYON

MGOMO wa siku mbili walioufanya wachezaji wa timu ya Yanga umeonyesha athari baada ya kulazimishwa sare ya bao moja dhidi ya African Lyon mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru na kushindwa kuishusha Simba kileleni.



Jumatatu na Jumanne ya wiki hii wachezaji wa mabingwa hao watetezi waligoma kushinikiza kulipwa mishahara yao ya mwezi Novemba hali iliyozusha sintofahamu kabla ya leo kubanwa mbavu na Lyon.

Mchezo huo ulikuwa wa taratibu ambapo dakika 45 za kipindi cha kwanza hakukuwa na shambulizi lolote la hatari kwa pande zote mbili licha ya Yanga kumiliki sehemu kubwa ya mchezo.

Mlinda mlango wa Yanga Deogratius Munishi 'Dida' kwa muda mrefu wa kipindi hicho alikuwa likizo kutokana na kukosekana kwa kashkashi baada ya Lyon kucheza zaidi nyuma na katikati ya uwanja.



Ludovic Venance aliipatia Lyon bao dakika ya 58 baada ya kupokea pasi ya Abdallah Mguhi ambaye alikuwa mwiba mkali upande wa kushoto ambao Haji Mwinyi alishindwa kabisa kumdhibiti.

Tambwe aliisawazishia Yanga kwa kichwa dakika ya 74 baada ya kumalizia krosi ya beki Juma Abdul kutokana na Lyon kushindwa kuokoa mpira ambao ulionekana hauna madhara.

Lyon iliwatoa Awadh Juma, Omari Abdallah na Thomas Morice na kuwaingiza Ludovic, Peter Mwalyanzi pamoja na Cosmas Lewis. Yanga iliwapumzisha Thaban Kamusoko, Mwinyi na Deus Kaseke na kuwaingiza Gofrey Mwashiuya, Emanuel Martin na Obrey Chirwa.

Yanga imefikisha pointi 37 alama moja nyuma ya Simba ambao kesho watacheza na JKT Ruvu na endapo watashinda wataongeza 'gepu' la pointi kufikia nne.