MWANAFUNZI AFAMAJI AKIOGELEA KRISMAS

Mwanafunzi wa darasa la tano wa Shule ya Msingi Sekei iliyopo jijini Arusha, Cliff Laiza (12) amekufa wakati akiogelea kwenye bwawa lenye kina kirefu katika Hoteli ya Kitalii ya Mount Meru iliyopo jijini Arusha katika sherehe ya Krismasi.



Tukio hilo siku ya krismas majira ya saa 12 jioni wakati Cliff na watoto wengine, walipokuwa wakiogelea katika hoteli hiyo, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Krismasi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Meneja wa Hoteli ya Mount Meru , alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na kusema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi na watatoa ufafanuzi baada ya polisi kukamilisha upelelezi wa tukio hilo.

Baadhi ya watoto waliokuwa wakiogelea na Cliff kwenye hoteli hiyo, walisema alihama ghafla kwenye bwawa la watoto na kwenda kuogelea bwawa linalotumiwa na watu wazima, ambalo wakati huo hapakuwa na mtu yeyote akiogelea, lakini ghafla hakuonekana tena hadi alipokutwa anaelea juu ya maji.

Babu wa mtoto huyo, Emanuel Meage alieleza kusikitishwa na tukio hilo na kueleza kuwa mjukuu wake aliaga kuwa anaenda kuogelea katika Hoteli ya Mount Meru yeye na wenzake. Hata hivyo, alisema alishangaa kusikia amekufa na kwa sasa wanamsubiri baba yake ili kujua ni hatua zipi wanazichukua kutokana na tukio hilo.