Yanga vs Azam, mechi ya kisasi leo

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara, Yanga leo wanawakaribisha Azam FC kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara huku wakiwakosa nyota wake watano ambao watashindwa kucheza mchezo wa leo.

Nyota watakaokosekana leo ni pamoja na Donald Ngoma na Amis Tambwe ambao wote ni majeruhi pamoja na Kelvin Yondani na Hassan Kessy ambao wote wana kadi tatu za njano.

Aidha, Yanga imepata pigo lingine jana baada ya kiungo wake, Thaban Kamusoko kuumia enka na hivyo kuukosa mchezo wa leo.



Hata hivyo habari njema kwa Yanga ni kurejea kwa beki wake wa kati, Vincent Bossou ambaye alirejea juzi kutoka kwao Togo alipokuwa na majukumu ya timu yake ya Taifa.

"Bossou ameingia juzi mchana na moja kwa moja alikuja mazoezini na kuungana na wenzake," alisema Kocha wa Yanga George Lwandamina.

Aidha, akizungumzia mchezo huo, Lwandamina, alisema itawabidi wapambane kupata ushindi.

"Ni mchezo muhimu sana kwetu.., tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri na suala la majeruhi hatupaswi kulifikilia.., Yanga ina wachezaji wengi wenye uwezo na naamini watakaopata nafasi ya kucheza wataipa matokeo mazuri timu," alisema Lwandamina.

Kwa upande wake, Kocha msaidizi wa Azam FC, Iddi Cheche, alisema pamoja na timu yake kutokuwa na nafasi ya ubingwa msimu huu, lakini watahakikisha wanaifunga tena Yanga ili kuendeleza rekodi nzuri ambayo wamejiwekea msimu huu kwa kuzifunga timu zote kubwa za Simba na Yanga.

“Wasijidanganye kwamba watashinda hata kama hatuna nafasi ya ubingwa lakini hatutokubali kutumika kama daraja kuwapa ubingwa tena msimu huu timu yetu ipo fiti,”alisema Cheche.

Azam inaingia Uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 4-0 dhidi ya Yanga waliopata kwenye mchezo wa mwisho wa timu hizo Januari mwaka huu walipokutana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.