Bandarini: Watumishi TRA,TBS wakalia Kuti Kavu Baada ya Kauli ya Waziri

SERIKALI imewataka baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), walioshirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Mapato (TRA), kupitisha makontena zaidi ya 100 bila kukaguliwa na shirika hilo katika Bandari ya Dar es Salaam, kujisalimisha haraka.



Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo. “Nimeanza kukusanya orodha ya majina ya watu waliosaidia kupitisha makontena haya na nikija nayo hawatapona,” alisema Mwijage.

Aliwataka wote wanaojijua kuhusika, kujisalimisha mapema na kutubu ili wasamehewe, kabla ya hatua hiyo. Makontena hayo yalipitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni bila ya kuthibitishwa na shirika hilo.
Waziri huyo pia aliitaka TRA kuacha kutoa makontena, bila ya shirika hilo kuthibitisha au kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini, kwa sababu mwenye mamlaka hiyo ni TBS.

Alisema watakaotubu kuwa walishiriki, waseme walishiriki vipi na lini, walishirikiana na nani na wataje sehemu yalikopelekwa makontena hayo ili serikali isaidie kukomesha hali hiyo. 

 #HabariLeo