WAZIRI MAKAMBA AAGIZA KUUNDWA KAMATI ZA AMANI NA MAZINGIRA KUSHUGHULIKA MIGONGANO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI KILOSA

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Mazingira na Muungano Mh January Makamba akiongozana na viongozi wa wilaya ya Kilosa akiwemo mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoi amekutana na wakazi wa kijiji cha Mbwade, Kata ya Madoto, Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro ambapo amezungumza  nao juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwa jamii huku akisisitiza juu ya matumizi bora ya ardhi kwa wakulima na wafugaji.



Waziri huyo ambaye anashughulikia mazingira amesikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho ambacho kinakaliwa na wakulima na wafugaji ambapo kwa kiasi kikubwa wameeleza changamoto kubwa ya mgawanyo bora wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji hasa katika kipindi cha ukame (mwezi wa 9,10 na 11) ambacho ndicho hasa kipindi cha migogoro.

Katika kushughulikia changamoto za mikwaruzano kati ya wakulima na wafugaji Waziri Makamba ameagiza kuundwa kwa kamati jumuishi ya amani ya kijiji ambapo ameahidi kuhakikisha kamati hiyo inapata mafunzo maalum ya upatanishi wa migogoro inayohusiana na rasilimali huku pia akiagiza kuundwa kwa kamati za mazingira kila kijiji/kata ambayo pia itapatiwa mafunzo maalum ya utunzaji wa mazingira hasa katika maeneo yenye ukame.

Katika ziara yake pia Waziri alifika katika kijiji cha Twatwatwa kata ya Parakuyo na kujionea changamoto wanazokumbana nazo wafugaji hasa kipindi cha kiangazi na kuwaasa kushiriki katika zoezi la uhakiki wa mifugo ili kuirahisishia kuweka mipango sahihi ya kuwasaidia.