Mtuhumiwa ‘panya road’ azindukia mochwari Dar

MTOTO aliyetambuliwa kwa jina la Isack Ernest (16) anayetuhumiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi cha uhalifu cha ‘panya road’ amezinduka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam.



Ernest, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumo na mkazi wa Buza, anayedaiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi hicho, alidhaniwa amekufa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuwaibia mali zao.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Gilles Muroto alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna vijana watatu wamekufa katika eneo la Mbagala na baada ya kufika eneo la tukio waliwakuta vijana hao wakiwa na hali mbaya.

Kamanda Muroto alimtaja mmoja aliyejulikana kwa jina la Kelvin Nyambocha (14) kuwa alikufa baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi na kwamba kabla ya mauti kumkuta alifuatana na wenzake kwa ajili ya kwenda kuangalia tamasha la muziki wa Singeli lililofanyika Mbagala Zakhem. Kijana mwingine Selemani Hamis (16), mkazi wa Kilingule, alifariki akiwa chumba cha upasuaji katika hospitali ya wilaya Temeke. 

#HabariLeo