PUTIN ASITISHA MKATABA WA NYUKLIA KATI YA URUSI NA MAREKANI

Urusi imesitisha mkataba wake na Marekani kuhusu kutupwa kwa madini ya ziada ya plutonium ambayo yanaweza kutumiwa kuunda silaha, ishara ya kudorora kwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye ushawishi mkubwa duniani.



Kupitia agizo rasmi, Rais Vladimir Putin ameituhumu Marekani kwa kuunda "kikwazo cha kutishia utathabiti, kwa kuchukua hatua zisizo za kirafiki" dhidi ya Urusi.

Bw Putin alisema Urusi imelazimika kuchukua "hatua za dharura kulinda usalama wa taifa la muungano la Urusi". Moscow imetoa masharti ya kutimizwa na Marekani kabla ya kurejelewa kwa mkataba huo.
Chini ya mwafaka huo wa mwaka 2000, kila taifa linapaswa kuangamiza tani 34 za madini ya plutonium kwa kuyachoma kwenye vinu vyake.

Mpango huo ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kupunguza silaha za nyuklia.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema tani 68 za madini ya plutonium ambazo zingeangamizwa "zinatosha kuunda silaha 17,000 za nyuklia". Pande zote mbili zilikuwa zimetia saini upya mkataba huo mwaka 2010.

Kwingineko, Marekani nayo imetangaza kwamba itasitisha mazungumzo na Urusi kuhusu mzozo Syria.
Marekani imesema Urusi haijatimiza masharti yaliyoafikiwa chini ya mpango wa kusitisha mapigano kwa muda mwezi jana, ambao umesambaratika.
Urusi imesema hatua hiyo ni ya kusikitisha na badala yake ikailaumu Marekani kwa kujaribu kuiwekea lawama Urusi.

#BBC