Ripoti ya mkataba wa Lugumi, Polisi yafika kwa Ndugai

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Projestus Rwegasira amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Bunge ya kuhakikisha mfumo wa vifaa vya utambuzi wa alama za vidole unafungwa katika wilaya za kipolisi 108 nchi nzima kwa muda wa miezi mitatu.



Zabuni ya kufunga na kusambaza mashine hizo za utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi ulifanywa na Kampuni ya Lugumi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo Naghenjwa Kaboyoka, aliwathibitishia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa ripoti hiyo tayari imekabidhiwa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kaboyoka alisema ripoti hiyo baada ya kukabidhiwa kwa Spika Ndugai ataipitia na baadaye kuiwasilisha kwa kamati hiyo ya PAC.

Juni 30, mwaka huu, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya kuahirisha Bunge la Bajeti aliiagiza serikali kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa ajili ya kuwadhibiti wahalifu na kuitaka Kamati ya PAC ifuatilie suala hilo.

Dk Tulia alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa yenye utata ya kuhusu zabuni yenye thamani ya Sh bilioni 37 ya kufunga mashine hizo katika vituo vyote vya Polisi baina ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited iliyotolewa mwaka 2011.

#HabariLeo