Theluji ya Mlima Kilimanjaro hatarini kutoweka

Theluji ya mlima kilimanjaro iko hatarini kutoweka kutokana na kushamiri kwa tatizo la uharibifu wa mazingira ambalo linasababishwa na shughuli za kibinadamu za kukata miti hovyo na kuchoma misitu ambapo takwimu zinaonyesha barafu iliyokuwa imetapakaa kwenye safu ya mlima huo imepungua kutoka mita 4500 hadi kufikia mita 1500 kwa sasa.

mlima kilimanjaro


Tatizo la uharibifu wa mazingira katika hifadhi za msitu unaozunguka hifadhi ya mlima Kilimanjaro umesababisha theluji  iliyokuwa imetapakaa  katika safu ya mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika kuyeyuka kutoka mita  4500 hadi kufikia mita 1500.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Bw.Saidi Meck Sadick amesema tatizo hilo la uharibifu wa mazingira kama halitadhibitiwa mapema kuna hatari ya theluji ya mlima Kilimanjaro kuyeyuka kabisa ifikapo mwaka  2025 na hivyo kuathiri shughuli za utalii.

Amesema wananchi  wanakata miti hovyo, kuchoma misitu kwa wingi na kwamba hali hiyo ambayo imeanza kuleta athari katika mlima Kilimanjaro kutokana na kuongezeka kwa ukame ambao umesababisha baadhi ya wilaya kukumbwa na baa la njaa  kutokana na  mvua kutonyesha kwa wakati.

Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa umoja wa dini  mbalimbali waliokutana mjini Moshi kujadili masuala ya utawala bora ,uchumi na suala la uharibifu wa mazingira msaidizi wa Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Moshi Padre Deogratius Matiika amesema kwa sasa wameanzisha mpango wa kuhamasisha waumini wa dini zote kupanda miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchini.

Nao baadhi ya wadau wa mazingira katika mkoa wa Kilimanjaro wanasema hali kwa sasa bado siyo ya kuridhisha kutokana na kuongezeka kwa joto kali ,na kwamba suala la utunzaji wa mazingira katika mkoa wa Kilimanjaro linatakiwa kuwa ajenda ya kudumu.