ANAANDIKA GOSLISTEN MALISA: HILI LA MAAFA BUKOBA, DR.SLAA AMEPOTOKA.!

By Malisa GJ,

Nimesoma maelezo ya Katibu Mkuu wa zamani wa CHADEMA Dr.Wilbroad Slaa juu ya hatua ya serikali kutumia fedha za misaada za wahanga wa Bukoba kutoka kujenga miundombinu ya serikali kama ofisi za idara na taasisi za serikali, mashule, barabara etc.



Dr.Slaa ameunga mkono hatua hiyo ya serikali. Katika maelezo yake aliyoyatoa kwa Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Kilimanjaro Ndg.Kibona Dickson, Dr.Slaa amejieleza kwa kirefu sana kwanini anaunga mkono hatua hiyo ya serikali ambayo wananchi wameitafsiri kama utapeli. Maelezo ya Dr.Slaa yana hoja mbili kubwa:

1. Hoja ya kwanza ya Dr.Slaa ni kile kinachoitwa katika ethics "Lesser evil". Yani yanapotokea makosa mawili na ukahitajika uchague moja basi unachagua lenye nafuu zaidi. Dr.Slaa anasema ni heri serikali itumie pesa hizo kuwajengea wananchi miundombinu kuliko kuwatelekeza kabisa.

Ametumia mifano miwili kutetea hoja hiyo:

Mfano wa kwanza, ni maafa yaliyotokana na mvua mkoani Shinyanga wilayani Kahama, ambapo Rais Kikwete aliwaahidi wahanga kuwajengea nyumba lakini Rais Magufuli akaja kufuta ahadi hiyo. Kwahiyo Dr.Slaa anaona kuliko serikali iwaahidi tena wananchi "ahadi hewa" ya kuwajengea, ni bora iseme ukweli kuwa itashindwa kujenga badala yake itajenga miundombinu tu.

Mfano wa pili, Dr.Slaa katumia wa mafuriko ya Kilosa mkoani Morogoro. Amesema wahanga wametelekezwa kwa zaidi ya miaka 10 bila msaada wowote licha ya ahadi kedekede za serikali kuwasaidia. Dr.Slaa anasema serikali iliwapa wahanga hao viwanja vya kujenga lakini vikavamiwa na viongozi wa serikali ngazi ya mkoa, wilaya na kijiji na kujigawia.

Kwa mujibu wa Slaa ni bora serikali iseme ukweli kuwa haitaweza kuwajengea wananchi kuliko kuwapa matumaini "hewa" au kuwaahidi halafu ikashindwa kutimizs. The theory of lesser evil.!

2. Pili Dr.Slaa amesema si jukumu la serikali kujenga makazi ya watu waliopata maafa, kazi ya serikali ni kujenga miundombinu tu. Na miundombinu ikijengwa itarahisisha zoezi la wananchi kujijengea makazi yao kuwa rahisi.
Dr.Slaa ametumia mfano wa jimbo moja huko Canada anapoishi kwa sasa kutetea hoja yake. Anasema nchini Canada katika Jimbo la Alberta, Mji wa McMurray, watu zaidi ya 70,000 walikumbwa na janga la moto uliokuwa unapelekwa kwa mwendo kasi mkubwa wa upepo. Watu hao waliokolewa lakini moto huo uliteketeza za nyumba zao.

Dr.Slaa anasema "Tulichangishwa kwa hiari na Red Cross, shule, Mamlaka za miji na Mitaa kwa njia mbali. Lakini, fedha zote hizo zilienda kujenga miundombinu, na huduma ya dharura ya muda mfupi kama nilivyoeleza juu. Wananchi waliopoteza nyumba zao walielekezwa kutumia " Insurance" zao" ili kufidiwa nyumba zao zilizoteketea kwa moto.

#MyTake:
Napenda niseme kwa kifupi kuhusiana na tamko hili la Dr.Slaa.

#Mosi: Dr.Slaa aelewe kwamba uovu hauwezi kutumika kuhalalisha uovu. Yeye ni Mkristo na amewahi kuwa kiongozi wa dini hivyo anafahamu kuwa dhambi haiwezi kutumika kutakatisha dhambi. Kama wananchi wa Kahama na Kilosa walidhulumiwa, kutapeliwa au kupewa ahadi hewa na serikali haiwezi kuwa kigezo cha kuhalalisha wananchi wa Bukoba nao kutapeliwa.

Ningemuelewa Dr.Slaa kama angetumia mifano ya Kahama na Kilosa kuionya serikali kuwa isijaribu tena kufanya ujinga wa aina hiyo badala ya kutumia mifano hiyo kuhalalisha utapeli wa serikali. Kwa mfano Dr.Slaa angeweza kusema "Tunajua namna serikali ilivyowaahidi wahanga wa Kahama na Kilosa kisha kuwatelekeza, kwahiyo tunaitaka serikali ya Magufuli isifanye yaliyofanywa na serikali iliyopita maana wananchi hatutakua tayari"

Lakini Dr.Slaa kusema serikali ilishawahi kuwatapeli wahanga wa Kahama na Kilosa bila kuwajengea nyumba wala miundombinu, kwahiyo ni bora iwajengee hata miundombinu hawa wa Bukoba, ni kauli ya kukata tamaa.
Ni sawa na kusema unakubali mwizi aje akuibie kisa tu hajajeruhi mtu. Kwamba una historia ya kuibiwa na kujeruhiwa kwa hiyo huyu aliyekuja kukuibia tu bila kujeruhi unamuona ni wa "maana zaidi" kuliko hao walikokua wakikuibia na kukujeruhi. Hii si sahihi hata kdg. Two wrongs never make it right.!

#Pili, Dr.Slaa amesema si JUKUMU la serikali kuwajengea watu makazi. Kwamba wananchi wanapaswa kujenga makazi yao wenyewe na serikali ijenge miundombinu. Hoja hii ya Slaa ingekua sahihi kama serikali ingekua inatumia pesa zake yenyewe na sio pesa za wafadhili.

Serikali ina mfuko wa maafa, ni vizuri pesa za mfuko huo zingetumika kukarabati miundombinu badala ya kutumia pesa hizi za msaada. Pesa za msaada zimewanga wahanga "specific" kwahiyo kupindisha matumizi yake ni utapeli. Hata ujumbe uliokua unatolewa na serikali wakati wakiomba misaada hiyo walisema "changia kusaidia WAATHIRIKA wa tetemeko Bukoba". Ukisoma ujumbe huo utaona kwamba msaada huo ulielekezwa kwa waathirika na sio kujenga miundombinu. Hakuna tangazo lolote lililosema "Changia kujenga miundombinu iliyoharibika Bukoba". Hakuna.

Sasa kama ujumbe ulikua ni "Changia waathirika Bukoba" leo pesa hizo zimepelekwa kwenye miundombinu, Dr.Slaa haoni huu ni utapeli? Katika kanisa nalosali tuliamua sadaka zote za jumapili moja zipelekwe Bukoba kusaidia wahanga. Sasa je, unadhani waumini wanajisikiaje kuambiwa sadaka yao waliyoitoa kwa ajili ya wajane, yatima, wazee na wahanga wengine zimepelekwa kujenga miundombinu?

#Tatu, Mwalimu wangu huyu wa siasa Dr.Slaa anajaribu kutumia mfano wa Canada kwa matatizo ya Tanzania anasahau kwamba hizi ni nchi mbili tofauti, zenye maendeleo tofauti, tamaduni tofauti, aina ya uongozi tofauti, na hali ya kiuchumi tofauti. Huwezi kuwaambia watanzania wajenge makazi yao wenyewe kisa huko Canada walijenga wenyewe.

Slaa anakiri kwamba Canada wananchi wengi wamekatia bima (insurance) nyumba zao na walipopata majanga walilipwa na makampuni hayo ya Bima. Lakini je hapa Tanzania ni watu wangapi wamekatia Bima nyumba zao? Katika majiji makubwa kama Dar, Mwanza na Arusha ni asilimia ndogo sana ya watu wana Bima za nyumba, sembuse Bukiba?

Hata magari tu kuna watu wanakatia Bima ili kuepuka usumbufu wa askari barabarani, na sio kulinda gari lake. Kwa kifupi hatuna elimu ya kutosha ya masuala ya Bima na umuhimu wake. Wengi wanaona kama ni kupoteza hela tu. Sasa Dr.Slaa anawezaje kujustify hoja yake kuhusu Bima huku akijua wazi suala la bima kwa nchi yetu ni changamoto?

Kwa kifupi niseme tu kuwa Mwalimu wangu huyu wa siasa, na kiongozi wangu wa zamani ninayemheshimu sana ameteleza kuhusu suala hili la maafa Bukoba. Amekosea na pengine atahitaji kuwaomba radhi watu wa Bukoba.

Serikali inapaswa kutoa pesa zote ilizochangisha kusaidia waathirika wa maafa ya Bukoba, na ni LAZIMA ishinikizwe pesa hizo ziwafikie walenga (Kwa njia mbalimbali. Si lazima wapewe cash, maana kuna watu wanaweza kuhoji modality ya kufikisha msaada huo kwa walengwa na kuwatoa wengine nje ya mjadala. Issue hapa sio cash. Issue ni msaada ufike kwa walengwa. Kama watapewa saruji, mabati, tofali etc lakini lazima msaada huo uwafikie). Then katika kujenga miundombinu serikali itumie fedha zake kutoka serikalini.(mathalani mfuko wa maafa), na sio hizi zilizochangwa na wafadhili.

Malisa GJ