Kikwete: Tatizo la ajira litakwisha |

RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jakaya Kikwete amewapoza wahitimu wa fani ya ualimu akisema wasikatishwe tamaa na tatizo la ajira katika sekta hiyo kwa kuwa ni suala la muda litakalokwisha muda mfupi ujao.

Kikwete


Dk Kikwete aliyasema hayo jana alipokuwa akiwajibu wahitimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa waliopaza sauti wakimtaka amuombe Rais John Magufuli afungue milango ya ajira katika sekta hiyo na sekta nyingine za umma.

Mmoja wa wahitimu hao (jina lake halikupatikana) alisema, “Inaumiza kuona wenzetu waliomaliza chuo hiki mwaka mmoja uliopita wakiendelea kusota mitaani na sasa tunaungana nao katika msoto huo.” “Ujumbe umefika,” Dk Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya nane ya chuo hicho yaliyofanyika jana katika viwanja vya chuo hicho mjini Iringa, alisema.

Aliwaambia wahitimu 952 aliowatunuku vyeti vyao katika fani nne za Shahada za Elimu kwamba tatizo la uchelewaji wa ajira kwao litakwisha baada ya muda mfupi kwa kuzingatia kwamba Taifa lina mahitaji makubwa ya walimu.

Kikwete aliyetumia dakika zisizozidi tatu kuzungumza na wahitimu hao wakati akifunga mahafali hayo, alisema ataufikisha ujumbe huo kunakohusika kama alivyoombwa. #HabariLeo