MTANZANIA AFUNGUA MGAHAWA SWEDEN NA KUVUNJA REKODI YA DUNIA

Mgahawa mkubwa unaotoa huduma za chakula cha Kitanzania unaomilikiwa na mpishi maarufu duniani, Issa Kapande `Chef Issa', umefunguliwa nchini Sweden na kuvunja rekodi ya dunia. Mgahawa huo ulizinduliwa na balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mh. Dora Msechu.



Balozi Msechu alimpongeza Issa Kapande na mkewe kwa kufanikisha kuwapo kwa mgahawa huo ambao umeweka rekodi kuwa mgahawa mkubwa kuliko yote ya Kiafrika katika nchi za Ulaya. Aidha, alimshukuru Torvald Brahm mwenyeji wa mji huo kwa kumuunga mkono Issa hadi kufanikisha ndoto yake ya kuwa na mgahawa wa kwanza wa Kiafrika katika mji wa Trollhattan utakatoa huduma ya chakula cha kitanzania.

Katika uzinduzi huo ambapo wenyeji wa manispaa hiyo akiwemo Meya na mwenyekiti wa Trollhattan, Paul Akerlund na msaidizi wake Peter Eriksson walikuwepo, balozi ambaye ndio kwanza ameanza kazi alielezea kufurahishwa na juhudi za Kapande.

Katika kazi yake ya upishi, amebahatika kuwapikia watu mashuhuri duniani, baadhi wakiwa Andrew Young, Mchungaji Jesse Jackson, Robert Mugabe (Rais wa Zimbabwe), Paul Kagame (Rais wa Rwanda), Benjamini Mkapa (Rais mstaafu wa Tanzania), Raila Odinga (Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya), Daniel Arap Moi (Rais Mstaafu wa Kenya), Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bi. Hillary Clinton na mumewe Bill Clinton, Mke wa Rais wa zamani wa Marekani Laura Bush.

Wengine ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, mwigizaji Chris Tucker, Rais wa zamani wa Afrika Kusini hayati Mzee Nelson Mandela, Koffie Olomide, Youssour ndour, Arsene Wenger (Kocha wa Arsenal ya England), Gianluca Vialli (nyota wa zamani wa Italia aliyewahi kuichezea na kuinoa Chelsea ya England), Rais wa Congo DRC, Joseph Kabila, Billy Gates na wengine wengi.

#BBC