Rais Lungu akataa biashara ya uswahiba bandari

RAIS wa Zambia, Edgar Lungu ameitahadharisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuwa Wazambia hawabanwi na urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili kupitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam, bali wanaendelea kufanya hivyo kutegemeana na ufanisi unaofanywa na mamlaka hiyo.



Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya vitengo vya bandari hiyo jana, Rais Lungu alisisitiza nchi yake itaendelea kupitisha mizigo kwenye bandari hiyo kama itaendelea kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa kuliko bandari zingine zilizoko katika ukanda wa kusini mwa Afrika. “Mimi na Rais Magufuli (John) tuna urafiki wa karibu, nchi mbili hizi pia zina urafiki wa muda mrefu, lakini Wazambia hawapitishi mizigo yao katika bandari hii kwa sababu ya urafiki wetu, bali wanachohitaji ni urahisi na uharaka wa kutoa na kusafirisha mizigo yao. “Pia hatuwaungi mkono kibiashara eti kwa sababu tu nchi mbili hizi tuna uhusiano mzuri, bali tunaangalia ni wapi ambako wanatoa huduma kwa haraka na kwa ufanisi...kwani naamini hata tusipowapa biashara undugu wetu wa damu utaendelea, lakini hatuendi kwingine tunakuja hapa kwa sababu ya ufanisi,” alisema Rais Lungu.

Rais huyo pia aliitahadharisha mamlaka hiyo kuwa wanatakiwa kuhakikisha kila siku wanabuni namna ya kuboresha huduma zao kwa kuwa kuna nchi jirani pia zinatoa huduma kama wanayotoa wao na ambao wangependa kupata biashara zaidi. 

#HabariLeo