Tanzania nzima kuwa na umeme ndani miaka 5

KUANZA kwa Utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (Turnkey III) ambao unafanywa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) utaifanya Tanzania Bara yote kuwaka umeme ndani ya miaka mitano.



Mradi huo utakaotekelezwa ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha, utaviunganisha vijiji vyote vya Tanzania Bara ambavyo havijapatiwa huduma ya umeme kuunganishiwa nishati hiyo.

Wakati akiahirisha Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema mradi huo utapeleka umeme katika vijiji 7,873 viliyoko katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara. Kwa mujibu wa Majaliwa, vijiji hivyo vitaanza kuunganishiwa umeme kuanzia mwaka huu wa fedha 2016/17.

Kati ya vijiji hivyo, vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi kutokana na nishati jadidifu. Waziri Mkuu alisema REA inafanya hivyo kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuvipelekea umeme kwa gharama nafuu kwa sasa.

Kwa mujibu wa takwimu za REA, hadi kufikia sasa jumla ya vijiji 4,395 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara sawa na asilimia 36 tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme.

Kama Tanzania ina vijiji 12,268, vijiji ambavyo vimeunganishiwa umeme hadi sasa ni vijiji 4,395, vijiji viliyokuwa vimebaki bila kuunganishwa na huduma ya umeme ni 7, 873 ambavyo Waziri Mkuu ametangaza kuwa vitaunganishiwa umeme ndani ya miaka mitano.


#HabariLeo