ASKARI WAFICHUA UFISADI WA SARE ZA MAGEREZA

Baada ya Rais John Magufuli kulipiga marufuku Jeshi la Magereza na majeshi mengine nchini kuruhusu askari wake kununua sare kwa watu binafsi, askari wa jeshi hilo wameibuka na kudai kuwa wamekuwa wanauziwa sare hizo kwa Sh 45,000.

Pia wamesema kofia na mikanda licha ya kuwa haiuzwi kwenye maduka ya watu binafsi, lakini upatikanaji wake pia ni wa shida, hali ambayo inawalazimu askari kutoa rushwa kwa wahifadhi bohari ili kupatiwa sare hizo.

Askari mbalimbali walisema licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa kulikemea suala hilo, walisema ni rahisi kushona kombati uraiani kwa kuwa vitambaa vinapatikana madukani, lakini kofia na mkanda ikichakaa askari analazimika kutoa pesa ili kupata mavazi hayo.

“Hizi kofia na mikanda inatolewa bohari ya jeshi, lakini kuupata huko mkanda au kofia lazima utoe rushwa kwa askari anayefanya kazi pale,” alisema mmoja wa askari
Wengi wa askari hao walisema kutokana na ugumu wa kupatikana na kofia na mikanda ya jeshi hilo, wengi wao wanaendelea kutumia kofia na mikanda waliyopewa wakati wanamaliza mafunzo.

Walisema kinachotolewa bure na jeshi hilo kwa sasa ni vyeo tu na sio sare nyingine yoyote. “Kofia hii ninayotumia pamoja na mkanda ni ile niliyopewa wakati namaliza depo (mafunzo) mwaka 2001,” alisema askari huyo ambaye ana miaka 15 sasa kazini na kuongeza, “Magereza wanachotoa bure kwa askari wao ni zile alama za cheo tu, vingine vyote vinavyohusu sare lazima askari ajinunulie.”



Wakati askari Magereza wanajinunulia sare, serikali imekuwa inatoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwahudumia askari hao.
Mfano, katika bajeti ya mwaka 2015/16 serikali ilitoa Sh bilioni 167.1 kwa jeshi hilo.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 67.7 zilitolewa kwa jeshi hilo kwa ajili ya matumizi mengineyo, Sh bilioni 97.7 kama mishahara na fedha za maendeleo zilizotolewa kwa polisi ni Sh bilioni 1.6 Askari mmoja ambaye yuko mkoani Simiyu alisema upatikanaji wa sare za Magereza kwa askari walioko mikoani ni mbaya, kwani wamekuwa wanalazimika kununua suruali na shati kati ya Sh 40,000 na 45,00 na viatu Sh 40,000.

“Juzi nilikuja hapo Dar es Salaam, nikawa na shida ya mkanda na kofia, nililazimika kutoa Sh 30,000 ambayo kofia niliinunua kwa Sh 10,000 na mkanda nilinunua kwa Sh 20,000,” alisema askari huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

Alipoulizwa anazipataje sare za jeshi hilo, alifafanua, “Sisi ukitaka sare unaenda kwa fundi unachukuliwa vipimo vya shati na suruali, unamtumia askari mwenzako wa Dar es Salaam anakununulia kitambaa na kukushonea, kisha anakutumia.” Alisema yeye tangu amalizmafunzo mwaka 2009 hajawahi kupewa sare yoyote