WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA (KIU) WAVAMIA WIZARA YA ELIMU KISA MIKOPO

Kundi la wanafunzi zaidi ya 100 wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) wametinga katika ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dar es Salaam wakitaka kufahamu hatma yao juu ya mikopo pamoja na fedha za kujikimu.



Hata hivyo, Naibu Waziri Stella Manyanya ameahidi kushughulikia tatizo la wanafunzi hao huku akiwaahidi leo kwenda katika chuo hicho kwa ajili ya kuzungumza nao na kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo.

Wanafunzi hao wamedai kuwa ni asilimia nane tu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuo hicho ndio waliopata mikopo huku wengine wakiwa hawajui la kufanya na hasa kwa kuzingatia gharama za ada ni kubwa.

Akizungumza baada ya kukutana na wanafunzi hao, Manyanya alikataa kuwasikiliza viongozi wa chuo hicho kwa alichosema wameshindwa kuheshimu na kufuata taratibu za kuonana na ofisi yake.

“Mimi ombi langu, tusiharibu yote naomba kesho (leo) nifike chuoni kwenu tukae pamoja, niweze kupitia pamoja hata kama mpaka jioni niko tayari kwa sababu ndio kazi yangu… lakini niseme mikopo inayotolewa haiangalii jina la chuo wala mwanafunzi,” alisema Naibu Waziri.

Naye Waziri wa Mikopo wa Serikali ya wanafunzi wa KIU, Baraka Haruni alisema kwa mwaka huu wamepokea jumla ya wanafunzi 1,486, lakini awali majina ya wanafunzi waliopaswa kupewa mikopo yalikuwa 354 na baadaye yalipunguzwa hadi kufikia 121.

Alisema pamoja na Naibu Waziri kuahidi kushughulikia, wanawasiwasi wa kukosa mitihani inayoanza Jumatatu, kwani kuwa hawajalipa ada.