SERIKALI YAFAFANUA UAMUZI WA KUZUIA USAFIRISHAJI WANYAMA HAI NJE

Dar es Salaam. Serikali imetoa ufafanuzi wa uamuzi wake wa kuzuia biashara ya usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa lengo la kupanga vizuri biashara hiyo kwa faida ya Serikali na wafanyabiashara wenyewe.



Ufafanuzi huo umetolewa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe katika kikao alichokiitisha wizarani hapo na wafanyabiashara wa wanyamahai wa makundi ya wadudu, vyura, mijusi, ndege, nyani na tumbili ambao walitaka kupata ufafanuzi wa hatma ya biashara yao kutoka serikalini.

Katika risala iliyosomwa na kiongozi wa wafanyabiashara hao, Adam Warioba kwa Waziri Maghembe, aliiomba Serikali kutoa ufafanuzi wa hatma ya biashara yao iliyofungiwa ambayo imekuwa tegemeo pekee katika kuendesha maisha yao huku wakitaka kujua hatma ya wanyama hai waliohifadhiwa na gharama zao walizolipa serikalini.

Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa Serikali kufungia biashara hiyo kwa wafanyabiashara hao, Profesa Maghembe amesema wanyama hai wengi kutoka nchini Tanzania wamekuwa wakisafirishwa nje ya nchi bila ya kufuata utaratibu maalum ikiwemo vibali vya kukamata na kuwasafirisha wanyama hao jambo ambalo limekuwa likiikosesha Serikali mapato mengi.

#Mwananchi