Shule za mihula 3 kufutiwa usajili

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imesema itazifutia usajili shule zote binafsi, ambazo zitabainika kukiuka agizo la serikali la kuzitaka shule zote nchini kuwa na mihula miwili ya masomo badala ya mitatu, ambayo imekuwa inafuatwa na shule zisizo za serikali.



Ili kutekeleza azma hiyo, wizara hiyo imewaagiza wakaguzi wa shule pamoja na maofisa elimu wa wilaya, kufanya ukaguzi katika shule binafsi zilizoko katika meneo yao; kubaini kama kuna shule binafsi zilizokaidi kutekeleza Waraka wa Elimu Namba Moja wa Mwaka 2015.

Kaimu Kamishna wa Elimu, Venance Manori alisema wizara yake ilitoa waraka huo ikiwa ni njia ya kukazia Waraka wa Serikali Namba 5 wa Mwaka 2012 ambao ulikuwa unaelekeza mihula ya masomo kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu, ifanane ili kuepusha usumbufu kwa walimu na kwa wanafunzi.

Waraka huo ulifafanua kuwa kila muhula utakuwa na likizo fupi na likizo ya mwisho wa muhula na siku za masomo kwa mwaka zitakuwa ni 194.

Pia waraka huo unataka siku za michezo ya Umitashumita na Umiseta kwa shule za msingi na sekondari, zifanane kwa shule zote. Lakini pamoja na kuwepo waraka huo, baadhi ya shule zisizo za serikali zimeendelea kufuata mihula mitatu.

Baadhi ya shule katika ripoti za wanafunzi za mwezi Desemba kwenda kwa wazazi, wameonesha kuwa mwaka ujao wa masomo utakuwa wa mihula mitatu na nyingine minne. “Wizara ilifanya utafiti na kujiridhisha kuwa haiwezekani shule zinazotoa elimu msingi kuwa na mihula mitatu, ndio maana tukataka nchi nzima tuwe na mfumo ambao unafanana ili kuepusha usumbufu kwa walimu na wanafunzi,” alisema Manori. 

#HabariLeo