Machinga wajimwaga mitaani wakimsifu Rais Magufuli

WAFANYABIASHARA ndogo maarufu Machinga katika Jiji la Mwanza, jana walilipuka kwa furaha huku wakizunguka mitaa ya katikati ya jiji, wakiimba nyimbo za kumsifu Rais John Magufuli huku wakimtakia afya na maisha mema kwenye uongozi.



Walifanya hivyo baada ya kutoa agizo la machinga hao na wa mikoa mingine, kutoondolewa katika maeneo hayo hadi pale mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa kwa kuwashirikisha machinga wenyewe. “Rais, Rais, Rais….tunakutakia maisha marefu uendelee kutuongoza Watanzania wanyonge 2020 tutakupa kura zote,” walisikika machinga hao jana alasiri baada ya kupata taarifa za uamuzi huo alioutoa Rais Magufuli akiwa Ikulu, Dar es Salaam.

Machinga Haruna Wambura ambaye ni mkazi wa Mji Mwema, alisema Rais Magufuli amefanya jambo jema la kuwarudisha katikati ya mji ambako watafanya biashara zao na kujiongezea kipato.

Dorica Mbisire wa Mahina Tambukareli ambaye pia ni machinga, aliupongeza uamuzi uliochukuliwa na Rais John Magufuli wa kuwarudisha mjini kuendelea na biashara zao. “Rais adumu milele na mwaka 2020 tutampa kura zote,” alieleza mwanadada huyo.

Aidha, gazeti hili liliwashuhudia baadhi ya machinga katika maeneo ya Makoroboi, wakianza kujigawia maeneo kwa kuweka alama na wengine wakichimba mashimo tayari kwa kurudisha vibanda vyao.

Katika uamuzi wake jana Ikulu, Rais Magufuli alimuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusitisha mara moja utekelezaji wa kazi ya kuwaondoa machinga katika Jiji la Mwanza pamoja na mikoa mingine mpaka hapo mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha machinga wenyewe.

Akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais Magufuli ameonya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie ngazi. 

#HabariLeo