TRA YAKOLEZA MAKALI YA ULIPAJI KODI



Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu kodi ili waweze kufahamu aina na madaraja ya kodi pamoja na umuhimu wa ulipaji kodi.



Mafunzo hayo yametolewa jana na Afisa wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, George Haule katika semina ya wakina mama wajasiriamali iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na kufanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo jijini hapa.

Haule amesema kuwa katika uanzishaji wa biashara ya aina yoyote jambo la kwanza na muhimu ni kujisajili katika mamlaka hiyo na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN - Number) itakayomuwezesha mfanyabiashara au mjasiriamali kuwa na biashara halali ambayo inalipiwa kodi kulingana na mauzo au faida ya biashara husika. “Tanzania ni nchi yetu na sisi Watanzania ndio tuna jukumu la kuitunza nchi hii, njia rahisi ya kuitunza nchi ni kulipa kodi stahiki ili kuinua pato la taifa kwa sababu kodi ndio chanzo kikubwa cha mapato ya nchi,”alisema Haule.

Haule ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inatumia mfumo endelevu wa ulipaji kodi kwa maana ya kila mfanyabiashara mdogo mwenye mauzo yasiyozidi 20,000,000 kulipa kodi ya mwaka kulingana na mauzo yake na mwenye mauzo yatakayozidi kiasi hicho cha fedha kulipa kodi ya mwaka kulingana na faida anayoipata katika biashara husika.