TWIGA WAKO HATARINI KUTOWEKA BARANI AFRIKA



Idadi ya twiga imepungua kwa karibu asilimia 40 barani Afrika tangu miaka ya 1980 katika kile kinachoelezwa kama ''kutoweka kimya kimya'' kunakosababishwa na uwindaji haramu na kuongezeka kwa maeneo ya kufanyia kilimo.



Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Red List, shirika linalofanya utafiti kuhusu wanyama walio katika kitisho cha kuangamia.Twiga, mnyama mrefu zaidi duniani, yuko katika hatari.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Mazingira, IUCN, idadi ya wanyama hao duniani imepungua na kufikia karibu 98,000 kutoka idadi ya twiga kati ya 152,000 na 163,000 iliyokuwepo mwaka 1985.

Ripoti ya shirika hilo inawaweka twiga katika hatari kubwa ya kutoweka kwa kuzingatia mienendo ya sasa ukilinganisha na ilivyokuwa awali. Kushuka kwa idadi ya twiga ambako hutokea sana katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara kunatokea kwa sehemu kubwa bila kutambuliwa.