ASKOFU MKUU ANGLIKANA : VIONGOZI KUBALINI KUKOSOLEWA

Viongozi kubalini kukosolewa- Askofu mkuu Anglikana Askofu mkuu wa kanisa Anglikan Tanzania Dkt. Jacob Chimeledya amewataka baadhi ya viongozi wanaokiuka ama kutokujua mipaka yao kiutendaji wajielimishe zaidi na kukubali kukosolewa badala ya kutumia nguvu kuwadhibiti watu wanaowakosoa na kusababisha malumbano ambayo matokeo yake huumiza watu wa chini wanategemea huduma kutoka kwao.

Ni katika misa takatifu ya kuliweka wakfu kanisa la mtakatifu Stefano azimio parishi ya Mtatana Dinari ya Kibaigwa ambapo pamoja na mambo mengine askofu Dkt. Jacob Chimeledya anatoa rai kwa viongozi wa umma kukubali kukosolewa na kujirekebisha hasa pale wanapokosea ili kujenga imani na jamii ambayo anadai inaathiriwa na malumbano baina ya viongozi hao na watu wanaowakosoa.

Baadhi ya waumini waliohudhuria misa hiyo takatifu wamewataka watanzania kuacha kutumia muda mwingi kufuatilia masuala ambayo hayana tija katika maisha yao ya kila siku ikiwemo kuperuzi katika mitandao ya kijamii muda wote badala yake wajikite kwenye kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Awali kabla ya kuanza kwa misa hiyo askofu Chimeledya alizindua choo cha kisasa kwa ajili ya watoto 216 wanaohudumiwa na shirika la Copasion Tanzania kanisani hapo huku akiitaka jamii kuepukana na tabia ya kusubiri msaada kutoka kwa wahisani ili kujiletea maendeleo kwani kwa kufanya hivyo ni kukaribisha umasikini ambao dini zote zinaupinga.