HALI YA UTULIVU YAREJEA NAMANGA MPAKANI MWA TANZANIA

HALI YA UTULIVU YAREJEA NAMANGA MPAKANI MWA  TANZANIA

Hali ya utulivu imerejea eneo la Namanga, katika mpaka wa Kenya na Tanzania siku moja baada ya raia wa Kenya kuandamana kupinga kile walichokitaja kama juhudi za serikali ya Tanzania za kuwalenga Wakenya wanaoishi na kufanya biashara nchini humo bila idhini.

Maafisa wa serikali ya Kenya na Tanzania wamesema kuwa wanashirikiana kutatua mzozo huo na kutoa wito kwa raia kuwa watulivu huku mzozo huo ukitatuliwa.

Serikali ya Kenya imesema kwamba hali ya utulivu imerejea.

Akizungumza na BBC, Kamanda wa polisi upande wa Kenya maeneo ya Kajiado ya kati, Eric Nteere, ametoa wito kwa wakaazi wa mji huo wakae kwa amani na serikali inazungumza na mamlaka za Tanzania na lengo la kutafuta suluhu ya kudumu.

Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania, Godfrey Chongolo mkuu wa wilaya ya Longido, inayopakana na taifa la Kenya, anasema kwamba shughuli za kuhakiki wananchi wa Tanzania pamoja na raia wa nchi za kigeni, ni za kawaida na sio mara ya kwanza kufanyika.

Alisisitiza kwamba Tanzania haina shida na mtu yeyote ambaye anaishi kwa kufuata utaratibu na sheria za nchi na ni lazima pande zote mbili zisimamie matakwa ya sheria.