ASKOFU GWAJIMA ATISHIWA KUUAWA

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema ametishiwa kifo na kundi la watu asiowafahamu.

Amesema kuwa watu hao waliomtumia ujumbe wa maandishi (SMS) kupitia simu yake ya mkononi na kuusambaza kwa watu, wengine walidai hatomaliza wiki hii iliyoanza leo.

Jana katika ibada yake, Gwajima alisema kuwa baada ya kuupata ujumbe huo alifanya maombi kwa ajili ya kuwafuta waliomtumia na kujua nini chanzo cha vitisho hivyo.

“Kuna Askofu anajiita Nabii mdogo juzi alikuwa anasambaza meseji anasema naona Gwajima anamaliza mwendo wake, nimeapa kwa jina la bwana yeye anayesema nitamaliza mwendo kwa nguvu za giza atamaliza yeye kwanza na siyo mimi” alisema Gwajima

Aliongeza kuwa chombo cha Mungu hakiwezi kwenda mbinguni kabla hakijamaliza kazi ya Mungu na kwamba ataendelea kuishi hadi pale Mungu atakapoona imetosha na siyo kwa vitisho vya binadamu.

“Jana nilikuwa namsaka aliyetuma meseji hiyo kwenye makorido ya kiroho, nikamuona, mimi nina agano na Bwana kwamba adui zangu wakija kwa njia moja wataondoka kwa njia saba, silaha zote zitakazokuja kwangu hazitofanikiwa, yeye ndiye atakayekufa siku ile ile aliyoipanga, siyo mimi” alisema.

Alisema anawajua waliojiandaa kufanya uovu huo dhidi yake na kwamba haogopi chochote, kwani yeye ni sauti ya Mungu na ataendelea kufanya kazi kwa nguvu kama alivyoagizwa na Mungu ili kutimiza kusudi lake hapa duniani.

“Unasema Gwajima atakufa, najua mipango yako yote, nawajua wale watu uliowaandaa kwa ajili ya kuuwa wapo wapi, wana umri gani na wanafanya kazi gani. Huyu anachekesha kweli, unataka Mungu akose sauti yake, watakufa wao waliotumwa na siyo mimi”

Gwajima alisema kuwa yeye na waumini wake wataendelea kuwa imara kwani wanamjua wanayemwamini na hawatishiwi na vitisho vya kifo kwa sababu Mungu atawashindia.

alinukuu maneno katika Biblia na kusema
“Nimepewa uwezo wa kuianza kazi hadi niimalize, mimi nina agano la bwana kwamba amwaminie yeye ataishi, na mimi nasema sintakufa bali nitaishi ili niyasimulie matendo makuu ya Mungu, sintaogopa silaha ya mchawi, iwe panga, iwe risasi haitofanikiwa mimi nitaishinda hadi niimalize kazi yangu.”

Askofu huyo amekuwa katika vita ya maneno na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam tokea alipotajwa katika sakata la orodha ya watuhumiwa wanaojihusisha na ama uuzaji au utumizi wa dawa za kulevya. Hata hivyo, Gwajima alijisalimisha polisi akapimwa na kubainika kuwa hajawahi kutumia dawa hizo na hivyo kuachiwa huru.

Vita hiyo ya maneno haikuishia hapo mpaka pale kiongozi huyo wa Mkoa wa Dar es salaam alipovamia kituo cha habari cha Clouds kulazimisha habari ya mwanamke aliyehojiwa akisema amezaa na Gwajima irushwe hewani ili kumchafua Askofu huyo wa kiroho.

Tukio la kuvamiwa kwa kituo cha Clouds lililoundiwa kamati ya uchunguzi na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye lilipelekea kutupwa nje kutokana na mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Dkt Magufuli, ambapo aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Harrison Mwakyembe kuchukua nafasi hiyo ya Nape ili kuiongoza Wizara hiyo.
HT @ TanzaniaDaima