PROF. MAGHEMBE: KUANZIA MAY MWAKA HUU MARUFUKU KUSAFIRISHA MKAA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ametangaza mabadiliko muhimu katika biashara ya mkaa nchini na kubainisha kuwa agizo la kutosafirisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda nyingine ili kunusuru misitu inayoteketea kwa kasi nchini litaanza kutekelezwa rasmi Julai.

Aidha, amepiga marufuku kuanzia leo usafirishaji wa mazao ya misitu ndani na nje ya nchi kwa kutumia nakala zisizo halisi, kuunga mkono Sera ya Uchumi wa viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano hakuna gogo litakalosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Maghembe  amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa 24 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, uliofanyika kwenye Ukumbi wa LAPF mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka kwenye Idara, Vitengo na Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya wizara hiyo.

“Kuanzia mwezi Julai hakuna ruhusa ya kutoa vibali vya kuhamisha mkaa kutoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine, mkaa utachomwa, utauzwa ndani ya wilaya kwa ajili ya matumizi ya Watanzania wanaohitaji nishati ya mkaa, lakini biashara ya mkaa ya kutoa Dodoma kwenda Dar es Salaam mpaka Zanzibar marufuku.

“Wamekata misitu yetu yote, mito yetu imekauka, tunashindwa kupata maji ya umwagiliaji kwa sababu watu wengi huko nje wanataka mkaa wetu, Tanzania jamani sio shamba la bibi, wale wote watakaotoa mkaa kutoka eneo moja hadi jingine kinyume na sheria hii watashuulikiwa kwa utaratibu wa uhujumu uchumi,” alisema Maghembe.

Alisema kwa upande wa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na Tanga vitaanzishwa viwanda maalumu vya kuzalisha mkaa ambao utauzwa kwa vibali maalumu katika mikoa mbalimbali nchini ambapo mkaa huo hautakuwa na athari nyingi za kimazingira kwa sababu utazingatia taratibu za uzalishaji endelevu.