Songea wazuiwa kufuga, kulima milima ya Lihanje

MKUU wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Pololet Mgema amepiga marufuku kufanyika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu kuzunguka safu ya milima ya Lihanje, ikiwemo kilimo na ufugaji ili mlima huo utumike kwa ajili ya hifadhi.

Akizungumza hivi karibuni na wakazi wa kijiji cha Litumbandyosi, Kata ya Litumbandyosi wilayani Mbinga mpakani mwa wilaya za Songea na Mbinga, Mgema alisema kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote kufanya shughuli zake katika safu ya milima hiyo ambalo limepandishwa hadhi na kuwa hifadhi.

Alisema kwa muda mrefu baadhi ya wananchi kutoka wilaya hizo mbili walikuwa na tabia ya kufanya shughuli za kilimo, ufugaji, uwindaji na ukataji miti kwa ajili ya mkaa kuzunguka milima hiyo jambo lililosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kupungua kwa vyanzo vya maji.

“Kuanzia sasa atakayekamatwa akifanya shughuli yoyote katika eneo lote la mlima Lihanje atakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria, lile eneo hivi sasa limetengwa kwa ajili ya hifadhi,” alisema DC Mgema.

Amewaagiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanasimamia vema agizo hilo la serikali kwa kuwadhibiti na kuwachukulia hatua watu watakaokaidi na kuendelea kufanya shughuli zao kuzungumza safu ya milima ya Lihanje.