MALISA GJ: MACHACHE NILIYOJIFUNZA TUKIO LA KUPIGWA MWANAFUNZI MBEYA.

By Malisa GJ,



1. Hakuna utaratibu rasmi wa kudeal na crisis serikalini wala hakuna protocal ktk kufanya maamuzi. Hakukuwa na sababu kwa mawaziri watatu kutoa tamko katika suala lile. Infact hata mmoja hakupaswa kutoa tamko. Lile halikua suala la kujadiliwa in Ministerial level.

2. Maamuzi ya serikali yamefanyika kwa mihemko bila kufuata utaratibu. Kwa mujibu wa sheria Waziri hana mamlaka yoyote ya kumfukuza chuo mwanafunzi. Kila chuo kina utaratibu wake kabla ya mwanafunzi kufukuzwa. Zipo kamati za nidhamu ambapo mwanafunzi huitwa na kusikilizwa kabla maamuzi kufanyika. Haki ya kusikilizwa ni ya kila mtu hata kama ameua. Cha ajabu walimu wale wa field wamefukuzwa bila hata kusikilizwa.

3. Serikali ya awamu ya 5 inafanya kazi kwa "mizuka" kama alivyosema Sugu. Wapo watoto wengi wanaopigwa kikatili kuliko huyo wa Mbeya lakini hakuna anayeshughulika nao kwa sababu tu hawajarekodiwa video. Serikali ilipaswa kuweka utaratibu wa kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanafunzi nchi nzima, sio kusubiri kupambana na tukio moja.

4. Tukio hili la Mbeya, linaweza kuchochea vitendo vya walimu kurekodiwa wanapotoa adhabu na hivyo kuzidisha uhasama baina wa walimu kwa walimu au walimu kwa wanafunzi.

5. Tukio hili linaweza kuchochea ari ya wanafunzi kutunishiana misuli na walimu wao. Kijana aliyepigwa mkoani Mbeya anadaiwa kumkwida shati mwalimu wake baada ya mwalimu kumpiga kibao. Hata Mkuu wa shule amekiri kuwa Mwanafunzi huyo alimkwida shati mwalimu wake na kumkaba koo mbele ya darasa.
Lakini hakuna anayezungumzia hili, wote wapo busy kulalamika mwanafunzi kaonewa. Kwa kawaida kosa moja halipaswi kuhalalisha kosa jingine. Ni kweli kuwa walimu walikosea, lakini mwanafunzi nae alikosea pia. Ni utovu mkubwa wa nidhamu kumshika shati mwalimu wako mbele ya darasa. Mwanafunzi huyu nae anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu, sio kuficha kosa lake kwenye makosa ya waalimu.

6. Walimu wengi hawazingatii kanuni za maadili katika kutoa adhabu kwa wanafunzi. Kwa mfano hakukua na sababu yoyote ya Mwalimu Frank kumpiga kibao mwanafunzi darasani, wakati kuna adhabu ya viboko. Na kama aligomea viboko angeweza kumpa visiki kadhaa vya kuchimbua ambavyo vingemfanya ajutie kosa lake.

7. Serikali haina utaratibu wa kumlinda mtoa taarifa. Kwa mfano Mhe.Mwigulu hakupaswa kudisclose jina la Mwalimu aliyerekodi video ile. Vinginevyo watu wengi watashindwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola hata kama wanao ushahidi, kwa sababu wataogopa kutajwa kama Mwigulu alivyomtaja mchukua video.

8. Ukaidi wa mwanafunzi huweza kuchochea walimu kutoa adhabu nje ya utaratibu. Ukitizama video ile mwanafunzi alipofikishwa "staff room" aliambiwa ashike chini ili aadhibiwe kwa viboko lakini akawa mkaidi, hali iliyopelekea walimu kumkata ngwara akaanguka na kuanza kumshambulia.

Lengo hapa si kuhalalisha adhabu ambayo walimu hao waliitoa, bali kuonesha kuwa mwanafunzi nae alichochea kufanyiwa ukatili. Hebu tafakari wewe ni mwalimu umempiga kibao mwanafunzi akakukunja shati, ukamuita ofisini ili umuadhibu, ukamwambia ashike chini akakugomea. Unaweza kuimagine hatua utakayochukua. Ukishatafakari hayo unaweza kuwahukumu walimu wa Mbeya day.

9. Social media zina nguvu kuliko vyombo rasmi vya habari. Nina uhakika kama tukio lile lisingerekodiwa, badala yake likawasilishwa kwa utaratibu rasmi wa malalamiko serikali lisingepewa uzito kama lilivyopewa baada ya kusambaa kwenye mitandao.

10. Viongozi wengi wa serikali ni "Fire fighters" sio "Fire preventers". Mojawapo ya sifa ya kiongozi ni kuwa "proactive" lakini viongozi wetu wengi ni "reactive". Hawana mkakati wa kuzuia crisis zisitokee, badala yake wanasubiri zikishatokea ndio wazitatue. Leo hii ukiuliza wizara ya elimu ina mkakati gani wa kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanafunzi mashuleni hawana, wanasubiri mwanafunzi mwingine afanyiwe ukatili ndipo wachukue hatua. Hii si sawa.!

Malisa GJ