MEXIME: KUCHEZA NA SIMBA NI KUJISUMBUA


Kocha wa Kagera Sugar Mecky Maxime ameilaumu Kamati ya masaa 72, kwa kuwapoka pointi tatu kwa madai ya kumchezesha beki Mohamed Fakhi mwenye kadi tatu za njano jambo ambalo halina ukweli.

Maxime amesema  maamuzi hayo yamemvunja nguvu na kumsikitisha sana kwa sababu hakuna ukweli wowote kuhusiana na hukumu hiyo ya kumchezesha mchezaji mwenye kadi tatu za njano.

“Inaumiza kiukweli kwa sababu hii inaonyesha kama vile TFF, wanataka kuipa Simba ubingwa kuna mambo mengi yasiyo takiwa kwenye mchezo wa Simba yanafanywa na viongozi wa timu hiyo lakini wanayafumbia macho hili ambalo siyo la kweli ndiyo wanalitolea maamuzi,” amesema Maxime.

Maxime amesema maamuzi hayo yamewakatili na kuwapotezea malengo yao ya kumaliza nafasi tatu za juu msimu huu kwenye ligi ya Vodacom ambayo kwasasa ipo katika hatua za mwishoni mwa msimu huu.

Amesema kwa namna hiyo watakuwa wanahofia kucheza na Simba kwa sababu hata wakiwafunga matokeo ya mchezo huo yanaweza kubadilishwa na kupewa pointi tatu hivyo nisawa na kupoteza nguvu.

“Ni vyema kama TFF na bodi ya ligi wakawapa Simba ubingwa kwani tunaona kuna dalilizote kutokana na upendeleo wanaopewa haipendezi ndiyo maana timu hizi zikifika kwenye michuano ya kimataifa hazifiki mbali kutokana na ubingwa wa mipango,” amesema.

Kamati hiyo iliipa Simba pointi tatu na kuifanya kuongoza ligi kwa kufikisha pointi 61, kabla ya mchezo wa leo dhidi ya Toto Africans na Yanga wamebaki kwenye nafasi ya pili wakiwa na pointi 56.