RAIS John Magufuli amefanya ukaguzi wa kushitukiza katika sehemu ya kukagulia mizigo na abiria ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam upande wa Terminal One na kuagiza maofisa wawili, waliotoa taarifa za uongo kwake Mei mwaka huu, wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Mei mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza mara baada ya kuwasili kwenye uwanja huo akitokea jijini Kampala nchini Uganda, ambako alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Museveni. Alitembelea kwa kushitukiza na kubaini kuwa mashine za ukaguzi (scanners) zilikuwa hazifanyi kazi.
Lakini jana baada ya kumsindikiza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye alikuwa akiondoka nchini baada ya ziara ya siku tatu, aliamua kufanya tena ukaguzi wa kushitukiza, na mara hii amebaini kuwa mashine hizo zinafanya kazi, baada ya kujionea yeye mwenyewe uhalisia wa namna mizigo inavyokaguliwa.
Hata hivyo, amemuagiza Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Paul Rwegasha kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wawili waliotoa taarifa za uongo alipofanya ukaguzi wa kushitukiza mara ya kwanza. “Leo kweli mashine zinafanya kazi na mimi nimeona, lakini wale walionidanganya mara ya kwanza nilipokuja, mkurugenzi hakikisha unawachukulia hatua,” alisisitiza Dk Magufuli, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana.
Rais Magufuli aliagiza maofisa hao, ambao kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, ni Lilian Minja na Novia Maduka ambao ni maofisa oparesheni wa JNIA, washushwe vyeo.#HabariLeo