Salamu za Julius Mtatiro kwa Rais JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI

HAPPY BIRTHDAY MR. PRESIDENT, JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI!
Na. Mtatiro J,
Mr. President,



Salaam!
Natambua kuwa umeongeza umri mkuu, aliye juu amekupa pumzi zaidi na tunaomba akupe zaidi na zaidi. Hongera sana.

Kupitia siku yako hii nataka nikukumbushe kuwa hatutaacha majukumu ya kukosoa, kupinga na hata kukataa kila jambo lenye chembechembe za UOVU ikiwa serikali yako italifanya au itataka kulifanya. Pia tutaendelea kukupongeza ikiwa kuna jambo umelifanya kwa weledi na maslahi ya wazi ya kitaifa na si chama chako. Miaka unayoongeza iwe kwa ajili ya kuwatendea haki watu wako, kuongoza serikali bila mipango ya kuvuruga na kuumiza vyama mbadala, viongozi na wanachama wake.

Mr. President, unao muda ukipenda, kurekebisha makosa yako na kila dalili za UDIKTETA kutoka kwa serikali yako na vyombo vyako. Unao muda wa kutosha kuweka vipaumbele sahihi kwa ajili ya taifa. Unao muda wa kutosha kujenga viwanda na kuweka miundombinu ili wananchi na taasisi za ndani na nje zikusaidie kuwekeza.

Mr. President, unao muda wa kutosha kuendeleza mambo mema yaliyoachwa na watangulizi wako. Huko nyuma tulikuwa na sheria mbaya ya vyombo vya habari/magazeti lakini haikuwa mbaya kama hii ambayo serikali yako inaleta. Kwa kifupi jitathmini na ujisahihishe. Miaka mitano ni muda mrefu sana, lakini ni muda mfupi kwelikweli na KUBOMOA NI RAHISI kuliko KUJENGA. Usibomoe misingi ya demokrasia changa iliyokuwa inaanza kukua, ukishaibomoa demokrasia hautakuwa na kitu mbadala cha kuweka, utaiingiza nchi matatizoni.

Mr. President, bandari inadorora, utalii haueleweki, sekta ya ujenzi inaporomoka na ajira hakuna! Watu walioko chini yako wasiendelee kukudanganya, kwamba unaungwa mkono sana na raia wa chini ati kwa sababu wewe ni mtetezi wa wanyonge. Hivi karibuji nilikuwa wilaya za Tarime, Musoma Mjini, Butiama, Bunda, Nyamagana, Misungwi, Shinyanga Mjini na Morogoro Vijijini. Huko kote wananchi wa chini wanalia, hali ya maisha ni ngumu mno. Wasaidizi wako wasikuwekee maneno ati hiki ni kipindi cha mpito na ati unanyoosha MFUMO, huu haunyoosheki brother, UNLESS utoe uongozi wa pamoja, uviachie vyombo vya habari vifanye kazi yake, kazi ya kufichua maovu yote, ya jamii na serikalini.

Mr. President, ili uongoze nchi kwa mafanikio, unavyo vyombo vya kikatiba. Kama kweli u mzalendo hebu iache polisi ifanye kazi kwa weledi wake na uwezo wao wote. Hebu liache Bunge lifanye kazi yake usiku na mchana. Iache mahakama ikae na uhuru wake. Jenga taasisi za taifa hili ili nazo zikujenge na kuonesha uimara na ukuu wa uongozi wako. Marais wote waliofanya ONE MAN SHOW hawakufika popote, walipigiwa sana makofi miaka miwili ya mwanzoni kisha wakakimbiwa na wananchi miaka mitatu ya mwisho. Sikuombei mabaya, nakukumbusha tu, kwamba cheo ni dhamana!

Halafu Mr. President, nasikia hata MITANDAO HII YA KIJAMII imekuchosha. Nimesikia tetesi eti unataka kuifuta!! Sasa watu kama mimi, wachokonozi, kina Malisa GJ na wengine, tutapataje nafasi ya kukukumbusha mchanga,na mchele wako?

Mr. President, yako mengi sana ya kukukumbusha kama kiongozi wetu mkuu wa nchi, mimi nimesema machache tu, wapo rafiki zako wanakasirika sana tukikukumbusha, sijui wewe binafsi hukasirika kiasi gani, lakini tatizo kubwa zaidi ni kwamba, haki ya kukukumbusha, haikopesheki, haichukuliki na haindoleki - hiyo ni haki ambayo tulizaliwa nayo na ili haki hiyo isikuguse ni lazima uwe hujaongoza ofisi uliyomo.

Nakutakia maisha marefu na nakukumbusha kuwa unao wajibu wa KUJENGA TAASISI IMARA katika nchi yetu, uongozi wa ONE MAN SHOW haukuwahi kufanikiwa kwa kudumu, kokote kule.
HAPPY BIRTHDAY OUR BELOVED PRESIDENT.
Mtatiro J,
Johannesburg,
29 Okt 2016.