Majaliwa aagiza upatikanaji wa wauaji wa watu waliokotwa mto Ruvu



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kuwabaini waliohusika na mauaji ya watu saba ambao miili yao iliokotwa pembezoni mwa mto Ruvu wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani, ikiwa kwenye mifuko ya sandarusi, ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao.



Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kuokotwa kwa miili hiyo Desemba 8, mwaka huu na kueleza kuwa matukio kama hayo, likiwemo la mjasiriamali kuuawa baada ya kutekwa mkoani Tabora, hayavumiliki wala kukubalika.

Alitoa maagizo hayo jana katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa kijijini Shelui wilayani Iramba mkoani Singida. Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.

Alisema, “Serikali kwa kushirikiana na Polisi, tena Waziri wa Mambo ya Ndani uko hapa (akimzungumzia Mwigulu Nchemba aliyekuwepo katika baraza hilo), tutaendelea na upelelezi ili wahusika wachukuliwe hatua kali.” Jana akihojiwa katika kituo cha televisheni cha Star TV, Mwigulu alisema uchunguzi umebaini kuwa miili saba iliyookotwa Bagamoyo ni ya wahamiaji haramu.

Miili ya watu sita ilikutwa Desemba 7, mwaka huu kando ya mto Ruvu wilayani Bagamoyo ndani ya mifuko ya sandarusi na ikiwa imewekwa mawe ili isielee kisha mifuko hiyo kushonwa kama mzigo wa mazao na kutupwa mtoni. 

#HabariLeo