MKANGANYIKO KESI YA 'MPEMBA' WA MENO YA TEMBO NA WENZAKE 6



Kesi ya kujihusisha na biashara ya meno ya Tembo inayowakabili watu sita akiwemo mfanyabiashara Yusuf Yusuf (34) maarufu ‘Mpemba’, imeendelea kuleta mkanganyiko mahakamani baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuelezea ni hatua gani zitafuata baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.



Kesi hiyo ambayo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas Simba kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwamba jalada lipo kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Kutokana na hoja hiyo, upande wa mawakili wa washitakiwa walidai kuwa kesi hiyo ilipokuja Novemba 16 mwaka huu, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi umekamilika na kwamba jalada linasubiriwa kupelekwa kwa DPP.

Hata hivyo, Hakimu Simba alisema kuwa jalada hilo kila linapokuja mahakamani linaleta mkanganyiko hivyo aliutaka upande wa mashitaka kuhakikisha kwamba katika tarehe nyingine kesi hiyo inapokuja, wawe na majibu ya kuridhisha kwamba baada ya upelelezi kuisha ni hatua gani zitafuata.

“Ni kweli kwamba mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, lakini upande wa mashitaka unatakiwa kueleza kwa nini mpaka sasa kama upelelezi umekamilika hakuna maelezo ni hatua gani zitafuatwa,” alisema Hakimu Simba.

Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 29 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Awali, kesi hiyo ilipopelekwa kwa mara ya kwanza upande wa Jamhuri ulidai unatarajia kuwapeleka washtakiwa hao katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama “Mahakama ya Mafisadi” kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Washtakiwa hao mbali na Yusuf ni Charles Mrutu (37) mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa (46) wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.

Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika shitaka la pili inadaiwa kuwa, Oktoba 26, mwaka huu, wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo va uzito wa kilo 13.85 vya thamani ya dola za Marekani 30,000 (Sh milioni 65.4).

Katika mashtaka mengine, inadaiwa Oktoba 27, mwaka huu, wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vya uzito wa kilo 11.1 na thamani ya dola za Marekani 15,000 (Sh milioni 32.7).

Aidha, Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vya thamani ya Sh milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Hakimu Simba alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu mashtaka yao kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliiahirisha hadi Desemba mosi mwaka huu.