Sababu za Joshua Nassari Kuipa Tano Serikali ya JPM

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ameipongeza na kuisifu Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada kubwa inazofanya katika kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali maeneo wanakotoka kote nchini.



Aidha, Nassari amewataka wabunge wenzake kushirikiana na serikali hiyo inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani sasa imeonesha dira ya maendeleo kwa wananchi wake na ameahidi kushirikiana nayo bega kwa bega kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu.

Nassari ametoa pongezi hizo jana mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa katika majumuisho ya ziara yake ya siku 10 ya kikazi mkoani Arusha.

Mbunge huyo aliyelazimika kuja nchini kwa dharura akitokea masomoni nchini Uingereza ili kumuwahi Waziri Mkuu, alisema ameridhishwa na hatua za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinazochukuliwa na Serikali.

Alisema ziara ya Waziri Mkuu mkoani Arusha, imesaidia kutibu majeraha na makovu makubwa yalitokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. “Kama kuna kiongozi ambaye hawezi kuunga mkono jitihada hizi za kuwaletea maendeleo watu wetu, atakuwa na matatizo,” alisema Nassari.

Alisema kitendo cha Waziri Mkuu kuweka mikakati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi ni ushahidi tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wananchi wa kawaida.

#HabariLeo