MVUA YASABABISHA VIFO, MAJERUHI NA WENGINE 170 KUKOSA MAKAZI


Takriban miezi sita baada ya kuathirika na tetemeko la ardhi, wakazi wa Bukoba wamefikwa na maafa mengine ya mafuriko yaliyosababisha watu 178 kuokolewa na nyumba zaidi ya 100 kuzingirwa na maji baada ya Mto Kanoni kufurika.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Migera, ambaye ni Diwani wa Kata ya Nshambya, Jimmy Karugendo amesema Kaya 40 zinahitaji msaada na miongoni mwa wakazi hao, wapo ambao awali waliathirika na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10 mwaka jana.

Kwa mujibu wa Mbunge wa kuteuliwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo, amesema mafuriko hayo yamesababishwa na mkondo wa maji kuzibwa.

Akitoa mfano wa eneo la Omukigusha ambalo ni miongoni mwa, maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko, ambalo kulikuwa mashamba ya miwa na mkondo wa maji, lakini sasa limegezwa makazi ya watu.

Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu bungeni, alisema tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera lilisababisha vifo vya watu 17, majeruhi 252 na nyumba 840 kuanguka. Nyumba zilizopata ufa ni 1264.

Wakati huo huo, Mkoani Arusha usiku wa kuamkia jana, mvua ilisababisha kifo cha mtu mmoja na familia zaidi ya 30 kunusurika katika Mtaa wa Ilkiurei, Kata ya Kiranyi, Wilayani Arumeru.

Katika hatua nyingine, Mkoani Tanga mvua imesababisha kifo cha mtoto aliyeangukiwa na ukuta, huku mwingine akijeruhiwa.