Sumaye kunyang'anywa Shamba



WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefuta hati tano za ardhi zilizokuwa zikimilikiwa na mfanyabiashara mwenye uraia wa Uingereza, Hamant Patel aliyemilikishwa kwa udanganyifu, huku ikiagiza watu wengine wasio raia waliomilikishwa ardhi kujisalimisha mara moja.

Aidha, wizara hiyo kupitia Ofisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Kinondoni imemuandikia notisi Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ya kulifuta shamba lake lililopo Mji Mpya eneo la Mabwepande, Dar es Salaam. Kauli hiyo imetolewa na Waziri William Lukuvi. Wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu uhakiki wa ofa za viwanja za Manispaa ya Jiji na Halmashauri.

Akizungumzia kuhusu kufutwa kwa hati tano zinazomilikiwa na Patel ambaye pia ni Wakala wa Kampuni ya Toyota Mwanza katika mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu, Lukuvi alisema wamebaini kuwa mtu huyo alimilikishwa ardhi kwa kutumia vyeti vya kughushi vinavyoonesha ni mzaliwa wa Tanzania.

Alisema hata hivyo walifanya uchunguzi na kupata taarifa kutoka Idara ya Uhamiaji kuwa mtu huyo ni raia wa Uingereza na anaishi nchini kwa kutumia kibali cha Daraja la Kwanza A ambacho kinaisha mwakani. “Nimeagiza Takukuru wafanye uchunguzi ili kubaini kama kuna maeneo mengine ambayo mtu huyu amenufaika nayo kama mzawa. Pia uchunguzi ufanyike ili kubaini wote walioshiriki hadi mtu huyu akamilikishwa ardhi,” alisema Lukuvi.
Akizungumzia kuhusu shamba la Sumaye, Lukuvi alisema shamba hilo walitoa notisi kwa kuwa halikuendelezwa kwa muda mrefu na kwamba serikali inafanya kazi bila kumuangalia mtu au cheo chake.
#HabariLeo