Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Kenya (COTU), Bw. Francis Atwoli alisema anaikubalia kasi ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa na kuwataka Watanzania wamuunge mkono badala ya kulalamikia kasi kwani wao wanatamani mwakani aende kugombea kwao katika uchaguzi mkuu ujao.
Magufuli |
“Ninawasihi wanaTUCTA suala la rushwa msilipe nafasi. Mpambane nayo kwa sababu kule kwetu imeota mizizi. Muungeni mkono Rais Magufuli, badala ya kulalamika kuwa kasi yake ni kubwa mno. Mnasema eti ana spidi sana, mkiona taabu mtuazime japo kwa mwaka mmoja ili aje atunyooshee mambo kule kwetu,” alisema huku akishangiliwa.
Aliwataka wahimize uhusiano uliopo baina ya vyama vya wafanyakazi, waajiri na Serikali iliyopo madarakani na kuwataka wadumishe umoja miongoni mwa viongozi na wanachama mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
“Msiruhusu mgawanyiko wa makundi baada ya uchaguzi sababu hauwasadii wafanyakazi ambao ni wanachama wenu. Mmeona madhara ya kuendeleza makundi kule nchini kwetu, msiruhusu hayo yatokee hapa,” alionya. TUCTA inatarajiwa kufanya uchaguzi wake kesho (Alhamisi, Novemba 24, 2016) na kuchagua uongozi mwingine utakaongoza kwa kipindi cha miaka mitano. Uchaguzi wa mwisho ulifanyika 2011.