Wanafunzi wa Udaktari (KCMU-Co) Watelekezwa

Moshi. Madaktari wanaosoma Shahada ya Uzamili chini ya udhamini wa Serikali katika Chuo Kikuu cha Kilimanjaro Christian Medical (KCMU-Co), hawajalipiwa ada kwa miaka miwili.


Zaidi ya madaktari 500 wapo kwenye makundi mawili; la kwanza likiwa ni la Shahada ya Uzamili wanaolipiwa na Wizara ya Afya na la pili ni madaktari wanaosomea shahada ya kwanza. Chuo hicho ambacho ni miongoni mwa vyuo vikuu vya Tumaini kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kipo ndani ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Vyanzo mbalimbali vimedokeza kuwa Serikali inadaiwa zaidi ya Sh3.5 bilioni, zikiwa ni ada na posho za wanaosomea shahada ya uzamili na ada kwa wanaosomea shahada ya kwanza ya udaktari.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangala alipoulizwa jana, alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo bila kuwa na taarifa za kutosha na za uhakika.

Hata hivyo, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Egbert Kessy alithibitisha chuo hicho kuidai Serikali na kwamba, wakati wa kuhitimu ukifika itawalazimu kuzuia vyeti vya madaktari hao.

#Mwananchi