Clinton aongoza kwa zaidi ya kura 2m dhidi ya Trump


Uongozi wa aliyekuwa mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton dhidi ya Donald Trump wa Republican katika kura za kawaida umeongezeka hadi kura milioni mbili. Rais Mteule Bw Trump alishinda uchaguzi huo wa urais uliofanyika tarehe 8 Novemba kwa wingi wa kura za wajumbe na ataapishwa Januari.

Matokeo ya Uchaguzi Marekani


Lakini kura za kawaida zinaendelea kuhesabiwa, wiki mbili baadaye, na kura za Cook Political Report zinaonesha ana kura 62.2m naye Bi Clinton 64.2m.

Hii ni mara ya tano kwa mgombea kuongoza kwa kura za kawaida lakini akashindwa uchaguzini kwani kura za wajumbe ndizo hutumiwa kuamua mshindi.

Mwaka 2000, mgombea wa Democratic Al Gore aliongoza dhidi ya George W Bush kwa karibu kura 544,000. Baada ya mvutano wa muda mrefu mahakamani, Mahakama ya Juu mwishowe iliamua mshindi wa urais baada ya kumkabidhi Bw Bush ushindi katika jimbo la kushindaniwa la Florida.

Mwaka huu, Bi Clinton alipata kura nyingi katika majimbo kama vile California lakini Bw Trump alishinda majimbo ya kushindaniwa, na kupata kura nyingi za wajumbe.

Mfumo wa kura za wajumbe humfaa zaidi mgombea ambaye anashinda, hata kama kwa kura chache, katika majimbo mengine dhidi ya yule anayeshinda kwa kura nyingi katika majimbo machache.

Kundi la wasomi, mawakili na wataalamu wa data pia wanajaribu kumshawishi Clinton na watu wake wajiunge na juhudi za kuchunguza matokeo katika majimbo matatu kubaini iwapo kulikuwa na uingiliaji wa mitambo ya kompyuta ya kuupigia na hesabu kura na watu kutoka nje.

Wanashangaa ni kwa nini Bi Clinton alionekana kutofanya vyema katika wilaya zilizotumia kompyuta kupiga na kuhesabu kura ikilinganishwa na maeneoa mbayo watu walipiga kura halisi za karatasi na mitambo ya skana ya kuhesabu kura.

Lakini maafisa wa kampeni wa Clinton hawajaonyesha nia yoyote ya kutaka kura zihesabiwe tena.

Mgombea wa chama cha Green Party, Jill Stein, anachangisha pesa za kupigania kura zihesabiwe upya katika majimbo hayo ya Michigan, Wisconsin na Pennsylvania ambayo Bw Trump alishinda.


Hayo yakijiri Donald Trump kwenye hotuba yake Siku ya Kutoa Shukrani amewahimiza raia wa Marekani kuunga mkono juhudi zake za "kujenga upya nchi" na kuponya makovu baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.

Chanzo: BBC